Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ametembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia nchini humo.

Akizungumza na Watumishi wa Ubalozi jijini Riyadh, Balozi Mulamula amewataka kuzingatia ulinzi wa taswira ya nchi yao hasa kwa kuzingatia mienendo ya maisha yao na kauli zao pia.

“Chochote mnachofanya ndio sura na kioo cha Jamhui ya Muungano wa Tanzania huku, nawaombeni sana kuzingatia hilo, japo ni kweli kwa mienendo yenu hatuwaingilii lakini hamna budi kujua kuwa nyie ni taswira ya nchi yetu huku,” alisema Balozi Mulamula.

Balozi Mulamula pia amewataka watumishi hao kuhakikisha wanafuata na kuzingatia misingi na kanuni za utumishi wa umma licha ya kutekeleza majukumu yao nje ya Tanzania.

Pia amewataka Mabalozi na watumishi walioko katika balozi za Tanzania kuendela kuwa walezi wa Watanzania popote walipo na kuwa tayari kuwasaidia pale watakapohitaji msaada kutoka katika balozi hizo.

Waziri Mulamula yuko nchini Saudi Arabia kwa ziara ya kikazi kufuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwana Mfalme, Mtukufu Faisal bin Farhan Al Saud, alioutoa mwezi Machi 2021 alipotembelea Tanzania na anataarajia kurejea nyumbani tarehe 13 Machi 2022.   

Katika ziara hiyo Waziri Mulamula ameambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki , kituo cha Uwekezaji nchini na Chama cha cha wafanyabiashara na wenye viwanda nchini (TCCIA).

Smollett atupwa jela kwa kudanganya Polisi
Ahmed Ally awashambulia walioipokea RS Berkane