Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limekubali kijadili mapendekezo yaliyotolewa na umoja wa mameneja wa klabu kubwa barani humo ya kufuta sheria ya bao la ugenini katika michuano ya ligi ya mabingwa na Europa League kuanzia msimu ujao wa 2019/2020.
Kaimu katibu mkuu wa UEFA Giorgio Marchetti, amethibitisha pendekezo hilo kuingizwa kwenye ajenda zitakazojadiliwa kwenye mkutano mkuu wa shirikisho hilo, utakaofanyika baadaye mwaka huu.
“Pendekezo lao tumelipokea na kwa bahati nzuri litakua ni sehemu ya ajenda zitakazojadiliwa kwenye mkutano mkuu, tuwaachie wahusika na kuona kama watapitisha pendekezo la kufutwa kwa sheria hiyo,” alisema kaimu katibu mkuu wa UEFA Giorgio Marchetti.
“Wao wanaamini ni sheria kandamizi kwa timu ambayo hutolewa mashindanoni kwa bao la ugenini, lakini bado ni mapendekezo yao, tumeyaheshimu na ndio maana tumeamua kuyaingiza kwenye ajenda za mkutano mkuu wa UEFA,” aliongeza.
Kaimu katibu mkuu wa UEFA Giorgio Marchetti
Sheria ya bao la ugenini katika michuano ya vilabu barani Ulaya ilianza kutumia mwaka 1965, kwenye michuano ya kombe la washindi ambayo kwa sasa ndio ligi ya mabingwa barani humo.
Mkutano wa mwaka wa umoja wa mameneja wa klabu kubwa barani Ulaya ulifanyika mwanzoni kwa mwezi huu, na kuhudhuriwa na Massimiliano Allegri (Juventus), Carlos Ancelotti (Napoli), Unai Emery (Arsenal), Paulo Fonseca (Shakhtar Donetsk), Julen Lopetegui (Real Madrid) Jose Mourinho (Manchester United), Thomas Tuchel (Paris St Germain) pamoja na aliyekua meneja wa Arsenal Arsene Wenger.