Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana leo Jumapili, baada ya mashambulizi ya Israel katika ukanda wa Gaza kuwaua watoto 8 na kuharibu majengo yaliyokuwa na ofisi za vyombo vya habari.
Hapo jana vikosi vya Israel viliushambulia ukanda wa Gaza, ikiwa ni siku ya sita ya urushaji mabomu katika eneo hilo la Palestina linalodhibitiwa na kundi la Kiislamu la Hamas ambalo nalo lilijibu kwa kufyatua maroketi.
Wakati Baraza la Usalama likijiandaa kukutana, jeshi la Israel limesema hii leo kuwa limeyalenga makaazi ya kiongozi wa juu wa kundi la Hamas.
Msemaji wa jeshi la Israel Brigedia Jenerali Hidai Zilberman amesema jeshi liliyalenga makaazi ya Yehiyeh Sinwar kiongozi mwandamizi wa Hamas katika eneo hilo na kuna uwezekano amejificha pamoja na wanachama wengine waandamizi.
Hamas imekiri kuwa wapiganaji wake 20 wameuawa tangu mapigano yaanze.