Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr amesema wizara ya sheria imechunguza madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa Novemba 3 na haijapata ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo yaliyotolewa na Rais Donald Trump.
Akiyazungumzia madai yanayotolewa na timu ya kampeni na kisheria ya Rais Trump, Barr amesema hadi sasa hawajapata ushahidi wowote kuhusu udanganyifu katika kiwango ambacho kinaweza kuyaathiri matokeo yaliyompa ushindi Joe Biden.
Barr amesema kufuatia kuwepo kwa madai kwamba kumekuwa na udanganyifu wa kimfumo na kwamba mashine zilipangwa mahsusi kwa ajili ya kuchakachua matokeo ya urais, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Sheria zimeyachunguza madai hayo, lakini hazijapata ushahidi wowote unaoweza kuyathibitisha.
Kwa muda mrefu Barr amekuwa akionekana kuwa mtiifu kwa Rais Trump tangu alipochukua nafasi ya Jeff Sessions mwaka 2018, lakini kabla ya uchaguzi vyombo vya habari viliripoti kuhusu Trump kutoridhishwa na mwenendo wake kwamba hakuonesha juhudi katika harakati za kiongozi huyo kuchaguliwa tena kuiongoza Marekani.
Mwezi uliopita, Barr aliwaamuru waendesha mashtaka wa shirikisho kuchunguza madai yoyote ya kuaminika ya udanganyifu, kabla matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2020 hayajathibitishwa na kuwataka wajiepushe na madai yasiokuwa ya kweli ambapo muda mfupi baadaye Trump aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba uchunguzi huo ni wa uongo.
Wakati huo huo, kiongozi wa wabunge wa chama cha Democratic katika Baraza la Seneti, Chuck Schumer amesema anahisi Barr ndiye anafuata kufukuzwa kazi na Trump, kwa sababu kiongozi huyo anaonekana kumtimua yeyote anayepingana na madai hayo.
Wanasheria wa timu ya kampeni ya Trump, Rudy Giuliani na Jenna Ellis wameapa kuendelea kuyapinga matokeo hayo mahakamani huuku timu hiyo ikifanya kila liwezekanalo kupitia vyombo vya habari, mahakama na majimbo kuzuia kuthibitishwa kwa Biden, Desemba 14.