Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24 Bungeni jijini Dodoma, na kuomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 2.98 trilioni za utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Wizara.
Bashungwa pia ametaja mambo tisa ambayo Wizara imepanga kuyatekeleza kwa mwaka wa fedha ambayo ni
1. Kuliimarisha Jeshi kwa zana na vifaa vya kisasa, mawasiliano na rasilimali watu.
2. Kuimarisha miundombinu mbalimbali katika Kambi za Jeshi na mipakani.
3. Kuendelea kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi kwa Wanajeshi ikiwemo
mafunzo, maslahi, huduma bora za afya na makazi.
4. Kuendelea kulijengea uwezo Jeshi la Kujenga Taifa kutoa mafunzo ya uzalendo,
ukakamavu, umoja wa kitaifa na stadi za kazi kwa vijana wa Mujibu wa Sheria na
wa Kujitolea.
5. Kuendelea kuimarisha Jeshi la Akiba.
6. Kuendeleza na kusimamia rasilimali za Jeshi ikiwemo miradi ya ujenzi hususan
Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa.
7. Kuimarisha mashirika na taasisi za utafiti wa masuala ya kijeshi, ikiwemo
uanzishaji wa viwanda katika sekta ya ulinzi (Defence industries) ili kuzalisha
bidhaa kwa matumizi ya Kijeshi na Kiraia.
8. Kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya
za Kikanda na nchi nyingine katika nyanja za kijeshi na kiulinzi.
9. Kuendelea kushirikiana na Mamlaka za Kiraia katika kukabiliana na majanga na
dharura inapohitajika.