Klabu ya Arsenal inakaribia kukamilisha usajili wa beki wa klabu ya Freiburg inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Ujerumani Caglar Soyuncu, kwa ada ya pauni milioni 35.
Wakala wa beki huyo kutoka nchini Uturuki, amefichua siri ya kinachoendelea baina ya Arsenal na klabu ya Freiburg ambayo imeridhia kumuachia Soyuncu.
Wakala huyo amesema tayari mazungumzo ya pande hizo mbili yameshakamilika, na wakati wowote Soyuncu anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya ili kukamilisha usajili wake wa kujiunga na manguli hao wa kaskazini mwa jijini London.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 22, msimu uliopita alikua kigingi katika safu ya ulinzi ya Freiburg, jambo ambalo lilimvutia mkuu wa kung’amua vipaji wa Arsenal Sven Mislintat.
Mpaka sasa Arsenal imeshakamilisha usajili wa Stephan Lichtsteiner akitokea kwa mabingwa wa soka chini Italia Juventus, na bado meneja mpya Unai Emery anasisitiza kufanya usajili mwingine ili kukiboresha kikosi chake.
wachezaji wengine ambao wapo njiani kusajiliwa na The Gunners ni beki wa Borussia Dortmund Sokratis Papastathopoulos na kiungo wa klabu ya Sampdoria Lucas Torreira.