Rais wa Belarus Alexander Lukashenko, ametangaza kuwa taifa hilo, limefunga mipaka yake na nchi za umoja wa Ulaya.
Lukashenko amesema ameliweka jeshi katika tahadhari kubwa na kufunga mipaka ya nchi hiyo na Poland na Lithuania.
“Sitaki nchi yangu kuwa vitani. Isitoshe, sitaki Belarus na Poland na Lithuania kugeuka kuwa maonyesho ya kijeshi ambako masuala yetu hayatatatuliwa. Kwa hivyo, leo mbele ya watu hawa wazuri kabisa, na wazalendo ninawaomba watu wa Lithuania, Poland na Ukraine – kuwakomesha wanasiasa wenu vichaa, msiruhusu vita izuke,” amesema Lukashenko.
Maafisa wa Poland pamoja na maafisa wa mpakani wa Lithuania wamesema kuwa hali katika mpaka na Belarus bado ni ya kawaida, wakisema wanasubiri kuona jinsi mabadiliko hayo yatavyotekelezwa.
Uamuzi wa Lukashenko unatilia mkazo madai yake ya kila mara kuwa wimbi la maandamano dhidi yake linachochewa na nchi za Magharibi.
Jana bunge la Ulaya lilipitisha kwa wingi azimio linalopinga matokeo rasmi ya uchaguzi na kusema halitamtambua Lukashenko kuwa rais halali mara baada ya muhula wake kukamilika Novemba 5.