Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans imeshindwa kutoa taarifa za kina kuhusu kurejea kambini kwa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison.
Morrison aliripotiwa kurejea nchini kwao Ghana baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Mzunguuko wa 19 dhidi ya Mtibwa Sugar uliopigwa Desemba 29, Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Ally Shaban Kamwe ameshindwa kutoa taarifa kamili kuhusu kurejea nchini kwa Morrison, ambaye jana Jumatatu (Januari 16) hakuwa sehemu ya kikosi kilichoivaa Ihefu FC, Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam.
“Morrison kuna ishu zake za kiofisi ambazo zinashughulikiwa. Naamini baada ya kukamilika Klabu itatoa taarifa rasmi kuhusu Bernard Morrison.”
“Hapa siwezi kusema Morrison atarudi kesho au keshokutwa wakati Kuna taratibu za kiofisi zinazoendelea kati ya Bernard Morrison na Uongozi wa Yanga”
“Taarifa Kuhusu yeye itatokea kwenye Ofisi ya Mtendaji Mkuu na Mimi Afisa Habari siwezi kuingilia Majukumu ya Makubaliano ya Kimakataba kati yake na Klabu.Siku ikifika ya Klabu kutoa Statement Mimi nitaitwa na nitaambiwa kazungumze hiki na hiki lakini mpaka sasa hivi hajafika na taarifa yake ni ya tofauti” amesema Kamwe
Morrison alirejea Young Africans mwanzoni mwa msimu huu baada ya mkataba wake wa miaka miwili na Simba SC kufikia kikomo.