Kikosi cha Mabingwa wa Soka nchini Uganda Vipers SC kimewasili salama jijini Dar es salaam, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wanne wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Simba SC.

Mchezo huo utachezwa kesho Jumanne (Machi 07), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku wenyeji Simba SC wakichagizwa na ushindi wa 1-0, walioupata nchini Uganda mwishoni mwa mwezi uliopita.

Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Wachezaji na Maafisa wa Vipers SC walionekana kuwa na furaha, huku kila mmoja akiamini wametua Tanzania kwa lengo la kulipa kisasi dhidi ya Simba SC.

Kocha Mkuu wa Vipers SC Roberto Luiz Bianch Pelliser amesema hawana budi kumshukuru Mungu kwa kuwasili Tanzania salama, na wana matumaini makubwa ya kushinda mchezo wa kesho dhidi ya Simba SC.

Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema amekiandaa vizuri kikosi chake na anatarajia kutumia mfumo zaidi ya mmoja, ili kuinyamazisha Simba SC, ambayo ilishindwa kufurukuta nyumbani ilipocheza dhidi ya Raja Casablanca mwezi uliopita.

KIKOSI CHA VIPERS SC KILICHOWASILI JIJINI DAR ES SALAAM TAYARI KWA MCHEZO DHIDI YA SIMBA SC

“Kesho tutakuwa na mifumo mingi na italenga maeneo yote kuanzia safu ya ulinzi hadi ushambuliaji, sihitaji kuona Vipers inakuwa timu ya mwisho tutafanya kama Raja Casablanca kushinda ugenini.” amesema Kocha Bianchi.

Vipers SC inaburuza mkia wa Kundi C ikiwa na alama 01, ikitanguliwa na Simba SC yenye alama 03, Horoya AC ipo nafasi ya pili kwa kumiliki alama 04, huku Raja Casablanca ikiongoza Kundi hilo kwa kufikisha alama 09.

Hatua ya Rais kuwafuta kazi Mawaziri yazua balaa
Ahukumiwa jela maisha kwa kumnajisi mtoto wake