Uongozi wa klabu ya Bishara United ya mkoani Mara umethibitisha taarifa za kuachana na kocha Amri Siad, na kuanza mpango wa kumsaka mrithi wake.
Kocha Amri amekua na matokeo mabovu tangu msimu huu wa 2019/20 ulipoanza mwishoni mwa mwezi uliopita, hali ambayo ilimpa wakati mgumu dhidi ya mashabiki wa Biashara ambao walihitaji kuona timu yao inafanya vyema.
Mwenyekiti wa Biashara United, Seleman Mataso amesema baada ya kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya JKT Tanzania kwenye mchezo wa jana uliopigwa uwanja wa Karume mjini Musoma, wameamua kuachana na kocha Amri Said.
Mataso amesema kikosi chao kitaongozwa kwa muda na kocha msaidizi, Omary Madenge huku uongozi ukiendelea kupambana kusaka mbadala ambaye ataweza kuwapa mafanikio msimu huu.
“Mashabiki wamemchoka na tukilazimisha aendelee kuwapo wanaweza kumjeruhi ikawa kesi nyingine, kwa hiyo timu itakuwa chini ya Msaidizi wake Omary Madenge,” alisema Mataso.
Hatua ya kuondoka kwa kocha Amri, inafikisha idadi ya makocha watatu waliofukuzwa tangu kuanz akw amsimu huu wa 2019/20 , awali Alliance FC ilimtimua Athuman Bilali ‘Billo’ huku Singida United nao wakimuonyesha mlango wa kutokea Fred Minziro.