Mabingwa Soka Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho (ASFC) wameanza maandalizi ya mchezo wa mzunguuko watatu wa Ligi Kuu dhidi ya Biashara United Mara.
Mchezo huo umepangwa kufanyika Jumapili Septemba 20, Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam na utakua wa kwanza kwa Simba SC kucheza nyumbani tangu walipoanza kutetea taji msimu huu 2020/21.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC Haji Sunday Manara amesema, kikosi chao kipo katika hali nzuri, na kinaendelea na maandalizi ya mchezo huo chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Sven Vandenbroeck.
Manara amesema hakuna namna nyingine ambayo watakwenda kufanya mbele ya Biashara United Mara zaidi ya kurejesha furaha kwa mashabiki wa timu hiyo, hasa baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Mtibwa Sugar, Septemba 12.
Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, amesema kikosi chake kimeanza kujiimarisha kuelekea mchezo huo na lengo ni kurekebisha makosa yaliyotokea katika mechi iliyopita.
“Mpira ni mchezo wa makosa, tumeshafunga hesabu za mechi iliyopita, sasa tunajiandaa kuikabili Biashara, akili zetu ni kuona tunapambana kusaka ushindi,” amesema Rweyemamu.
Mbali na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba SC walianza vizuri msimu huu kwa kupata ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Ihefu FC, Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Septemba 6.
Msimu uliopita Simba SC walipokutana na Biashara United Mara, Uwanja wa Benjamin Mkapa waliibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja, hali ambayo inachukuliwa kama chachu ya ushindani maridhawa ambao utaonekana kwenye mpambano wa Septemba 20.
Biashara United Mara inayonolewa na kocha kutoka Kenya Francis Baraza, imeshajikusanyia alama sita za VPL, baada ya kuzibanjua Gwambina FC na Mwadui FC, bao moja wa sifuri kila mmoja.
Michezo mingine ya mzunguuko watatu ya VPL itakayochezwa mwishoni mwa juma hili.