Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema huenda zaidi ya Shilingi Trilioni moja zikapatikana kwa mwaka kutokana na biashara ya kaboni na kutoa wito kwa wabunge kuhamasisha wananchi katika maeneo yao, kushiriki biashara hiyo kwa kupanda miti kwa wingi hatua itakayosaidia katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Jafo, ametoa kauli hiyo hii leo Februari 2, 2023 wakati akichangia Taarifa ya utekelezaji wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma Februari 01, 2023 huku akiwataka Wakala wa Huduma za Mistu Tanzania (TFS), kuhakikisha misitu yote itatumika katika biashara ya kaboni.
Amesema, miongoni mwa maeneo ambayo yameanza kunufaika na biashara ya kaboni ni pamoja na Halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi ambayo kwa wastani kwa mwaka inapata takriban sh. bilioni 2 hadi 3 hivyo ametoa hamasa kwa wilaya zingine kuhakikisha wanatunza misitu kwa ajili ya biashara hiyo.
“Niwaombe ndugu zangu wabunge tupitie kanuni na mwongozo wa kusimamia biashara ya kaboni hii itasaidia sana hasa jatika kuhakikisha maeneo yetu na kuona jinsi gani tunayaelekeza hasa katika suala zima la kuvuna hewa ukaa,” amesisitiza.
Aidha, amesema Waziri Jafo amesema biashara ya kaboni itagusa TFS ambao wana dhamana ya kuhifadhi misitu na kilimo (agro-forest) kwa wakulima wanaojihusisha na kilimo cha mikorosho, miparachichi na kahawa huku akiwapongeza wananchi kwa kuiunga mkono Serikali kwa kuchukulia ajenda ya kuhifadhi mazingira katika umuhimu wake kwa kuhakikisha wanapanda miti na kuitunza.
Awali, akichangia katika taarifa hiyo Mbunge wa Kuteuliwa, Liberata Mulamula ametoa wito kwa Serikali kuchangamkia fursa ya kupata fedha za mabadliko ya tabianchi zinazotolewa na nchi zilizoendelea kwa nchi zinazoendelea.