Mshambuliaji mpya wa Simba SC Jean Othos Baleke ameahidi kuendelea kupambana, ili kufikia ndoto zake za kufanya vizuri, kabla ya msimu huu kufikia kikomo.

Baleke ametoa kauli hiyo akiamini bado ana nafasi kubwa ya kuisaidia Simba SC kwa kufunga mabao muhimu ambayo yataipa alama tatu Klabu hiyo ya Msimbazi, inayoendelea kuufukuzia ubingwa, ikiachwa kwa tofauti ya alama sita na Young Africans yenye alama 56.

Mshambuliaji huyo amesema anatambua kwa sasa Mshambuliaji wa Young Africans Fiston Mayele ndio anaongoza kwa ufungaji wa mabao, na anamjua vizuri vizuri mtu huyo.

Amesema dhumuni lake ni kuhakikisha anakuwa sehemu ya wachezaji watakaofanya vizuri katika Ligi Kuu, hata kama hatofikia idadi ya mabao yaliyofungwa na Mayele, ambaye ni mpinzani wake tangu wakicheza Ligi Kuu ya DR Congo.

“Mayele tulikuwa na ushindani mkubwa sana wakati tukicheza wote Ligi ya DR Congo, mimi nikiwa TP Mazembe na yeye akiwa AS Vita, kitendo hicho kinanipa hamasa nipambane ili kufanya vizuri katika Ligi ya hapa Tanzania.”

“Ni kweli Ligi hii kwa sasa Mayele anafanya vizuri, ni moja kati ya washambuliaji wanaofanya vizuri, hivyo nataka kuwa sehemu ya watu watakaofanya vizuri, nitahakikisha kila kitu kinakuwa sawa.” amesema Baleke

Baleke alisajiliwa Simba SC kupitia Dirisha Dogo la Usajili akitokea TP Mazembe ya kwao DR Congo, ambayo mwanzoni mwa msimu huu ilimpeleka kwa mkopo Nejmeh SC ya Lebanon.

Tayari ameshacheza michezo miwili akiwa na Simba SC, akifunga bao moja dhidi ya Dodoma Jiji FC, iliyokuwa nyumbani Uwanja wa Jamhuri, Jumapili (Januari 28).

Biashara ya Kaboni kuineemesha Tanzania: Jafo
Taasisi za Dini zina mchango kuendelea amani: Rais Mwinyi