Beki wa kati kutoka nchini Ivory Coast Serge Pascal Wawa amesema anaiheshimu sana Simba SC, ambayo aliwahi kuitumikia kabla ya kutimkia Singida Big Stars mwanzoni mwa msimu huu.

Wawa aliitumikia Simba SC misimu minne mfululizo na kuwa sehemu ya kikosi kilichoipa mafanikio klabu hiyo katika Michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

Beki huyo anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Singida Big Stars kitakachoivaa Simba SC, katika mchezo wa Mzunguuko wa 22 wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kesho Ijumaa (Februari 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Wawa amesema daima ataendelea kuiheshimu Simba SC, lakini linapokuja suala la kazi atahakikisha anatimiza wajibu wake ili kudhihirisha ubora wa Singida Big Stars, iliyojipanga kumaliza nafasi za juu msimu huu.

“Naiheshimu Simba ila kwa upande wa kazi nikiwa uwanjani dakika 90 akili na nguvu zangu zinakuwa kuitetea timu yangu kupata alama tatu. Ndio maana nasisitiza utakuwa mchezo wa kuvutiwa.”

“Tunataka kuionyesha Simba sisi ni washindani na tunahitaji nafasi za juu na timu yetu tupo wachezaji wazoefu, ambao tutataka kulinda heshima yetu.” amesema Pascal Wawa

Wachezaji wengine ambao waliwahi kucheza Simba SC na wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Singida Big Stars kesho Ijumaa (Februari 03) ni Mshambuliaji Meddie Kagere na Kiungo Said Khamis Ndemla.

Homa uchaguzi TLS yaibua taswira mpya
Majaliwa asisitiza weledi, miiko utumishi wa Umma