Watu wawili wamefariki dunia visiwani Zanzibar akiwemo bilionea wa Russia, Igor Sosin ambaye alikutwa amefariki katika chumba cha hoteli ya Park Hyatt iliyopo mtaa wa Mji Mkongwe mjini Unguja.
Mwingine aliyefariki ni Nadra Abdulrazak Haji (3), mkazi wa Beit el Ras wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja ambaye alizama katika bwawa alipokuwa akiogelea na wenzake.
Sosin (53) alikuwa visiwani humo kwa ajili ya mapumziko ya mwisho wa mwaka sambamba na kufanya utalii, ambapo aliwasili Zanzibar, Desemba 17 akiwa ameambatana na mtoto wake aliyefahamika kwa jina la Taisia.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadh Juma Haji amethibitisha kutokea kwa kifo cha Bilionea huyo kuwa kilitokea usiku wa Desemba 23.
Kwa mujibu wa kamanda huyo siku ya kifo chake, Sosin alikuwa na mwanamke aitwaye Arafa Ramadhan Mpondo (23), mkazi wa Fuonim Zanzibar ambaye anadaiwa kuwa ni mpenzi wake aliyempata kwa njia ya mtandao.
Alisema baada ya kuhojiwa Arafa alieleza kuwa saa 5:45 usiku alimuona marehemu hayuko vizuri lakini akaamua kulala naye hadi asubuhi ambapo kulipokucha alimuamsha lakini hakuamka, ndipo alipotoa taarifa kwa uongozi wa hoteli kwa ajili ya hatua zaidi.
Kamanda ameeleza kuwa mwili wa marehemu ulipelekwa hospitali ya Mnazi Mmoja na majira ya saa 5:51 usiku kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na mwanamke huyo, bado anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano huku wakisubiri majibu ya uchunguzi wa kidaktari ingawa hadi sasa imebainika kuwa Bilionea huyo alikufa kifo cha kawaida.
Bilionea huyo mwanzilishi wa kampuni za Starik Hottabych na Modi za nchini Urusi anayeaminika kuwa na utajiri unaokadiriwa kuwa Dola Bilioni 18 (Sh 41.5 trilioni), alitambulika kupenda kuzunguka na boti baharini na kucheza mpira wa tenisi.
Kuhusu tukio la pili, Kamanda Awadh amesema nalo lilitokea Desemba 23 saa 17:30 jioni huko katika hoteli ya Zanzibar Beach Resort iliyopo wilaya ya Magharibi‘B’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja ambapo Nadra alipelekwa katika hospitali ya Al- Rahma kwa matibabu lakini alikuwa ameshafariki dunia.
“Japokuwa kifo kinapangwa na Mungu lakini kuna dalili za uzembe wa wazazi wake kwani haiwezekani mtoto wa miaka mitatu akaachiwa akaogelee bila ya uangalizi wa wazazi wake,” ameeleza Kamanda Awadh.