Serikali imetenga shilingi bilioni 16.5 ili kuweza kukamilisha zoezi la kufanya ukarabati wa hospitali 19 nchini katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Kauli hiyo, imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa viti Maalum, Esther Midimi.
Amesema, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ni miongoni mwa Hospitali kongwe 50, ambayo ilianza kutoa huduma kwa ngazi ya kituo cha Afya na mwaka 1989 ilipandishwa hadhi na kudai kuwa katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali itatenga fedha za ukarabati wa hospitali 31 zilizobakia ikiwemo hospitali ya Wilaya ya Meatu.
Katika swali lake la msingi, Mbunge wa viti Maalum (CCM), Esther Midimi alitaka kujua ni lini serikali itajenga Hospitali ya Wilaya katika halmashauri ya wilaya ya Meatu kwa kuwa hospitali iliyopo ina hadhi ya kituo cha afya na haikidhi mahitaji.