Serikali nchini, inaendelea kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kushirikiana na nchi mbalimbali duniani ili kukuza uchumi wa nchi kupitia fursa za biashara, uwekezaji na utalii zilizopo ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Felista Njau kuhusu umuhimu wa Serikali wa kuainisha nchi zenye fursa za biashara na uwekezaji, ili kukuza pato la Taifa.

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akijibu swali bungeni jijini Dodoma.

Amesema, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara za kisekta na Balozi za Tanzania imeendelea kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zenye manufaa kwa Taifa na kwamba Wizara inaandaa Mpango wa Kitaifa wa kutekeleza Diplomasia ya Uchumi utakaojumuisha Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kufikia malengo tarajiwa.

Mpango huo ambao unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Desemba 2023, pia unalenga kuhakikisha fursa za biashara, uwekezaji na utalii zinakuwa na tija zaidi kwa wananchi wa Tanzania na utajumuisha Sekta zote husika ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo muhimu ya kisekta yatakayo changia katika kukuza uchumi na pato la Taifa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akichangia hoja kuhusu Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi wakati wa kipindi cha maswali na majibu kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma.

Kuhusu mkakati wa utoaji elimu kwa wananchi kuhusu dhana ya Diplomasia ya Uchumi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax amesema Wizara inaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali.

Dkt. Tax amefafanua kuwa mpango mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi unaoandaliwa, pia utajumuisha utoaji wa elimu kwa umma kuhusu dhana hiyo, ili kuwawezesha wananchi kuielewa dhana hii na kuwawezesha kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali.

Simba SC ishindwe yenyewe Guinea
NIC watoa elimu huduma za Kidijitali