Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amesema tangu walipowasili mjini Conakry jana Alhamis (Februari 09) majira ya jioni, kikosi chao hakijapata matatizo yoyote.#

Simba SC Kesho Jumamosi (Februari 11) itacheza mchezo wa Mzunguuko wa kwanza wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Guinea Horoya AC, majira ya saa moja usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Ahmed amesema Kikosi cha Simba SC kiliwasili saa 11 jioni na kila kitu kinakwenda sawa kuelekea mchezo wa kesho utakaopigwa Uwanja wa General Lansana Conte.

Ahmed amesema Hali ya Hewa ya Mji wa Conakry ambako mchezo wa Simba SC na Horoya AC utafanyika, ni sawa na jijini Dar es Salaam hivyo wachezaji hawatapata changamoto yoyote inayohusiana na hali ya hewa.

Ahmed ameongeza kuwa kikosi kitafanya mazoezi ya mwisho leo Ijumaa (Februari 10) majira ya jioni katika Uwanja wa General Lansana Conte ambao utatumika kwenye mchezo wa kesho.

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu tumefika salama nchini Guinea jana jioni. Wachezaji walipewa mapumziko na watafanya mazoezi ya mwisho leo jioni kabla ya kesho kushuka uwanjani.”

“Kwa kweli hatukupata changamoto yoyote ya nje ya uwanja, baada ya kufika usafiri ulikuwepo tayari kutupeleka hadi hotelini tulipofikia kwa hiyo hali ni nzuri.” amesema Ahmed Ally

Mchezo mwingine wa Mzunguuko wa Kwanza wa Kundi C utachezwa leo Ijumaa (Februari 10) mjini Casablanca katika Uwanja wa Mfalme Mohammed V, kati ya wenyeji Raja Casablanca dhidi ya Vipers SC kutoka nchini Uganda.

Makusanyo ya Serikali yameongezeka: Waziri Mkuu
Ukuzaji wa Uchumi: Tanzania kutumia fursa ndani na nje