Mahakama ya Pennsylvania nchini Marekani imemshushia mvua ya kifungo cha kati ya miaka mitatu hadi kumi, mchekeshaji Bill Cosby mwenye umri wa mika 81, baada ya kumkuta na hatia ya kufanya unyanyasaji wa kingono na ubakaji dhidi ya msichana, miaka 14 iliyopita.
Jaji wa mahakama hiyo amesema Cosby amekutwa na hatia katika makosa matatu aliyoyafanya mwaka 2004, akimnyanyasa kingono na kumbaka msichana aliyetajwa kwa jina la Andrea Constand.
Mahakama pia imeamuru Cosby kusajiliwa kwenye orodha ya wanyanyasaji wa kingono na kwamba anapaswa kuhudhuria programu maalum ya kisaikolojia kwa kipindi cha maisha yake yote.
Kwa mujibu wa hukumu iliyosomwa mahakamani hapo, Cosby alimualika msichana huyo nyumbani kwake, kisha akamuwekea vidonge vya dawa za kulevya kwenye kinywaji chake kabla ya kuanza kumuingilia kwanza kwa kutumia vidole vyake.
Msichana Andrea Constand, alieleza kuwa kitendo hicho kilimtoa usichana wake, kumsababishia maumivu makali pamoja na matatizo makubwa ya kisaikolojia.
“Baada ya kunifanyia vitendo hivyo, nilipoamka sikua na uhakika wa nini hasa kilichonitokea ila maumivu yalisema kwa ukali. Aibu ilinijaa. Nilikuwa najishtukia na nilichanganyikiwa kiasi cha kushindwa kuirudia familia yangu au marafaki kwa hali ya kawaida kama nilivyozoea,” alisema.
“Nilijisikia mpweke sana kiasi cha kushindwa kumuamini mtu yeyote hata mimi mwenyewe. Hakika Bill Cosby alinitolea uzuri wangu, alichukua afya yangu ya ujana na kuiharibu. Alinifanyia unyang’anyi wa afya yangu na asili yangu pamoja na imani yangu kwa watu wengine pamoja na mimi mwenyewe,” aliandika mrembo huyo.
Utetezi mkuu wa Cosby ulikuwa ni pamoja na kwamba ukimya wa msichana huyo kwenye tukio hilo ilikuwa ni dalili ya kukubaliana na kilichokuwa kinafanyika, utetezi ambao Jaji aliutupilia mbali akisisitiza suala la kutumia vidonge vitatu vya rangi ya blu vilivyomlevya Andrea kabla ya kumfanyia unyama huo.
Mbali na Andrea, wasichana wengi walijitokeza mitandaoni kulalamikia vitendo vya unyanyasaji wa kingono katika miaka iliyopita walivyodai kuwa walifanyiwa na Cosby.
Mahakama pia ilitumia ushahidi huo katika kumpa adhabu Cosby.