Serikali Nchini, imesema lengo la kuwepo na Mifuko ya Bima ya Afya ni la kutaka Wananchi kuchangiana gharama za matibabu kabla ya kuugua, ili kuepusha familia hasa za masikini kwa kutumia fedha nyingi kugharamia matibabu.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel jijini Dar-es-Salaam wakati akiongea na Vyombo vya Habari, ili kuelezea mafaniko ya Sekta ya Afya katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema, “Serikali imefanikiwa kuboresha Sekta ya Afya kwa ujumla, changamoto kubwa iliyobaki ni namna ya kuwawezesha Wananchi kugharamia huduma za afya. ili kufikia dhamira ya Serikali ya Afya Bora kwa Wote ni lazima kuwa na mfumo endelevu na imara wa uchangiaji wa gharama za matibabu kabla ya kuugua.”
Aidha, Dkt. Mollel amesema Mwaka 2016 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulianzisha mpango wa bima ya afya kwa watoto walio chini ya miaka 18 (Toto Afya Kadi) kwa lengo la kuwezesha kundi la watoto kwa ujumla wao kujiunga kupitia shule za awali, msingi na sekondari ili kunufaika na mpango huo.
“Hata hivyo, pamoja na uhamasishaji uliofanyika kwa kupindi cha takriban miaka saba (7) bado mwitikio haukuwa wa kuridhisha kwani idadi ya watoto waliojiandikisha ilikuwa ni 210,000 kati ya lengo la watoto milioni 25 kwa kipindi hicho”. Amesema Dkt. Mollel.