Bodi mpya ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) imezinduliwa kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa Taasisi na uangalizi wa karibu katika matumizi ya fedha za umma  katika mahitaji mbalimbali.

Uinduzi huo umefanywa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji mjini Singida ambapo amesema Bodi hiyo itamsaidia Waziri wa Fedha na Mipango kupata ushauri wa kitaalam na hatimaye kutoa maamuzi yenye tija kwa Taasisi na Taifa kwa ujumla.

  “Bodi hii ya Ushauri inategemewa kutoa mchango wa mawazo na kitaalam yanayohusu uendeshaji  na uboreshaji wa Taasisi yetu ya TIA ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea duniani katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kiteknolojia, kisiasa na kijamii”, amesema Dkt. Kijaji.

 Aidha, ameongeza kuwa Bodi hiyo ina wajibu wa kujua ubora wa wanafunzi wanaohitimu katika chuo hicho ikiwa ni pamoja na ubora wa vyeti vyao kuendana na uwezo wao wa kufanya kazi katika fani walizosomea na kukabiliana na changamoto kwenye maeneo ya kazi.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania, Said Chiguma amesema Taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto ya uchache wa miundombinu kama vile kumbi za mihadhala, madarasa, maktaba na maabara za kompyuta ambavyo ni nyenzo muhimu katika utoaji wa elimu iliyo bora.

 Chiguma amesema ili kupunguza changamoto hizo, Taasisi inajitahidi kutenga fedha inazozikusanya ili kukarabati na kujenga majengo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha elimu na kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi.

 Taasisi ya Uhasibu Tanzania ni chuo cha Serikali ambacho kinatoa mafunzo katika fani za Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi wa Biashara, Uongozi wa Rasilimali Watu, Masoko na Uhusiano wa Umma pamoja na Uhasibu wa Fedha za Umma kuanzia ngazi ya Astashahada (Certificate), Stashada (Diploma)  na Shahada(degree)

IGP Sirro: Jeshi la Polisi limejipanga kutokomeza uhalifu nchini
LIVE: Rais Magufuli akihutubia wananchi Tabora