Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mej. Jenerali (Mstaafu), Hamis Semfuko imefanya ziara ya kikazi katika Pori la Akiba Kijereshi, lililopo Mkoani Simiyu.
Ziara hiyo, iliyofanyika Desemba 21, 2022 imelenga kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 25 na lango kuu la kuingilia wageni, ambapo pia ilikagua kituo cha kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu kilichojengwa katika kijiji cha Mwabayanda, Wilayani Busega,Mkoa wa Simiyu ambacho ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa miradi hiyo, Semfuko amesema TAWA imetekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga vituo vya vya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wananchi na mali zao zinalindwa dhidi ya wanyama wakali na waharibifu.
Aidha, Mwenyekiti huyo pia alipata wasaa wa kuzungumza na watumishi wa TAWA Kanda ya Ziwa na kusisitiza watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwa wazalendo.
Awali, Kamanda wa Kanda ya Ziwa, Gisela Kimario aliwasilisha taarifa fupi ya Kanda na aliwashukuru Bodi ya Wakurugenzi kwa kutenga muda wao na kufanya ziara fupi ya kikazi katika Kanda anayosimamia.
Hii inakuwa ni ziara ya kwanza ya kikazi ya Bodi ya Wakurugenzi- TAWA tangu walivyoteuliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Balozi Pindi Chana mnamo mwezi Septemba, 2022.