Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Bongani Mahlangu raia wa Afrika Kusini ameibuka na kuweka wazi kuwa anakuja nchini kwa kazi moja ya kuhakikisha anatoa burudani ya kumchapa kwa KO mpinzani wake Fadhili Majiha.
Hiyo ni kuelekea katika pambano la Royal Boxing Tour Ep 2 linalotarajia kupigwa Oktoba 28, mwaka huu kwenye Ukumbi wa PTA, jijini Dar es salaam.
Pambano hilo ambalo limeandaliwa na HB SADC Boxing Promotion ambapo pia Ibrahim Class anatarajia kupanda ulingoni dhidi ya Xiao Tau Su raia wa China wakati Nasibu Ramadhani Pacman anatarajia kupanda ulingoni dhidi ya Zolisa Baty wa Afrika Kusini huku Stumai Muki akitarajia kumvaa Loveleen Thakuur wa India.
Bongani amesema kuwa yeye anakuja nchini kwa kazi ya kuhakikisha Majiha hatoki kwenye mikono yake bila kupokea kipigo cha KO atakachoweza kumpa ili watu watambue kwa nini anaitwa profesa na aliweza kumpiga Tony Rashid kwa mara ya kwanza alivyokuja.
“Nategemea kuja Tanzania wiki ijayo nikiwa na timu yangu ya makocha wangu wawili, mashabiki waambie nakuja kufanya kazi ambayo hakuna anayetarajia kama itatokea hiyo Oktoba 28.
“Nataka niwaambie nilikuja nikampiga Tony Rashid na ndiyo nitakavyompiga Majiha halafu wao ndiyo wataelewa kwa nini Bongani ni Profesa, mazoezi ninayofanya ni kwa ajili ya kupiga KO na wala siyo jambo lengine, najua Majiha amejiandaa na ni bondia mzuri lakini wanatakiwa kujua kwamba nitampiga,” amesema Bongani