Viongozi mbalimbali wa nchi za magharibi, wameelezea matumaini ya kurejea kwa utulivu kufuatia kujiuzulu kwa waziri mkuu wa Uingereza Liz Truss, huku Boris Johnson akijipigia chapuo kuirejelea tena nafasi hiyo.
Rais wa Marekani, Joe Biden amesema kuwa ana matumaini Washington, itaendelea kushirikiana kwa karibu na London huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisema kuwa ana imani Uingereza itarejea haraka katika hali yake ya kawaida.
Mwenyekiti wa Kamati ya wabunge wa Conservative, inayohusika na uchaguzi wa viongozi, Grahma Brady, amesema chama hicho kitamchagua kiongozi wake mpya kufikia Oktoba 28.
Tayari kuna fununu kwamba waziri mkuu wa zamani Boris Johnson anakusudia kuwania tena nafasi hiyo huku baadhi ya wabunge ndani ya chama chake wakipinga wazo la kumrejesha madarakani wakidai kuwa bado anakabiliwa na uchunguzi wa kashfa iliyomwangusha.