Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeridhia ombi la upande wa Jamhuri la kumpeleka Mkurugenzi wa Kampuni ya kampuni ya kufua umeme (IPTL), Herbinder Seth mahakamani hapo Juni 14, 2021 ili kuieleza mahakama hiyo mazungumzo yao na mshtakiwa yalipofikiwa.
Ombi hilo limeridhiwa na Hakimu Mkazi Huruma Shaidi leo Juni 11,2021 baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Martenus Marandu kuieleza Mahakama kuwa wameshafanya mazungumzo na mshtakiwa Seth na Jumatatu watatoa mrejesho.
“Mheshimiwa, mshtakiwa aliandika barua kuhusu hatma ya shauri lake Juni 10, 2021, hivyo tumekubaliana kujielekeza kwenye barua hiyo na tunaomba muda ili tuweze kuifanyia kazi na kama itakupendeza kutoa amri ya kesi hii kuja Jumatatu ili tuitaarifu mahakama makubaliano yetu yamefikia wapi,” amesema Marandu.
Kufuatia taarifa hiyo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 14, mwaka huu na mshtakiwa amerudishwa mahabusu.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo, James Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP na Wakili wa kujitegemea, Joseph Makandege wao hawajaonesha nia ya kuandika barua kwa Mkurugenzi wa mashtaka nchini DPP hivyo kesi yao itaendelea kama kawaida na itatajwa Juni 17, mwaka huu.
Seth na wenzake wanadaiwa kati ya Oktoba 18 ,2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.