Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Camilius Wambura amesema Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu yeyote atakayeendelea  kujihusisha na vitendo vya uhalifu hususani wakati huu ambao Jeshi hilo linaendelea na Operesheni kali ya kupambana na vitendo hivyo.

DCI Wambura ameyasema hayo leo Juni 11, 2021 jijini Dodoma katika kikao kazi kilichowashirikisha Maofisa wa Makao Makuu ya Upelelezi na Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa nchini kwa lengo la kupanga mikakati ya kupambana na uhalifu  pamoja na kutathmini hali ya uhalifu nchini.

Amesema kuwa mtu yeyote amabaye anajihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja kwa kuwa mkono wa Jeshi la Polisi ni mkubwa  na kwa wakati huu hakuna upenyo wowote utakaoachwa kwa kuwa Operesheni inaendelea nchi nzima.

“ Wito wangu kwa wahalifu ni bora   watafute kazi nyingine ya kufanya kwa kuwa hatuna huruma kwa watu hao na Wananchi waendelee kutupatia taarifa zao ili tuhakikishe nchi yetu inaendelea kuwa salama,” amesema Wambura.

Kwa upande wake Naibu DCI, DCP Faustine Shilogile amesema Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Makao Makuu inaendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu na utoaji wa mafunzo kwa watendaji wa idara hiyo ili kuwa na wapelelezi wenye weledi ambao watasaidia kuharakisha upelelezi wa kesi zinazoripotiwa katika vituo vya Polisi.

Mtanzania aliyepanda Mlima Everest arejea nchini, aeleza siri ya mafanikio yake
Boss wa IPTL kupelekwa mahakama ya Hakimu Mkazi