Uongozi wa Klabu ya Brighton and Holve Albion umewatuliza Mashabiki wake kuhusu mustakabali wa Kiungo kutoka nchini Argentina Alexis Mac Allister, baada ya kuibuka mjadala kufuatia kiwango alichokionesha akiwa kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2022.

Mac Allister alikuwa chachu ya mafanikio ya Argentina kufanya vizuri kwenye Fainali hizo, hadi kutwaa Ubingwa wa Dunia kwa kuifunga Ufaransa juzi Jumapili (Desemba 18).

Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya England Paul Barber, amesema hawana shaka kuwa Kiungo huyo ataendelea kuwa sehemu ya kikosi chao kwa mujibu wa mkataba uliopo baina ya pande hizo mbili.

Amesema Mac Allister mwenye umri wa miaka 23, ana mkataba na Klabu ya Brighton and Holve Albion hadi Juni 2025, na pia wana nafasi ya kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja wakati wowote kuanzia sasa.

“Ataendelea kuwa hapa kwa mujibu wa Mkataba uliopo, tuna nafasi pia ya kumuongeza mwaka mmoja kwenye mkataba wake, hivyo niwatowe hofu Mashabiki ambao wameanza kuhisi huenda Mac Allister akaondoka, kutokana na kiwango kizuri alichokionesha Qatar,”

“Kuhusu uwezo wake tuliamini ipo siku angeishangaza Dunia na ndio maana alisajiliwa hapa, Mac Allister amezaliwa kwenye fainali ya mpira, baba yake aliwahi kucheza na Gwiji wa Argentina [Diego] Maradona, kwa hilo hatukuwa na shaka nalo kabisa,” amesema Barber.

Mac Allister alisajiliwa Brighton kwa mkopo Januari 2019 kwa ada ya Pauni Milioni 7, akitokea Boca Juniors ambayo baadae iliamua kumuuza jumla.

Rais Samia: Lazima tulipe mikopo
Karim Benzema aachana na Ufaransa