Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Hassan Bumbuli amerekebisha kauli aliyoitoa siku mbili zilizopita ya kutoutambua mchezo wa Jula 03, ambao utawakutanisha dhidi ya watani zao wa jadi Simba SC.
Bumbuli aliukana mchezo huo alipohojiwa na vyombo vya habari kwa kusema, tayari tarehe ya mchezo huo imeshapita na hawaufikiri tena, zaidi ya kuamini wamesaliwa na michezo minne kabla ya kumalizika kwa msimu huu 2020/21.
Amesema alichokua akikifanya kwenye mahojiano hayo ni utani, na kwa bahati mbaya wadau wa soka waliipokea vibaya kauli yake, hadi kuzua taharuki kubwa katika kona mbalimbali za vijiwe vya soka la Bongo.
“Mchezo wa watani wa jadi upo palepale tarehe Julai 03, kinachoendelea kwenye mitandao ya jamii ni mambo ya utani wa jadi lakini mchezo wetu dhidi ya Simba SC ni mchezo wa kiporo,”
“Kiporo ni cha kuchemsha au kupasha tu na kula ndo maana sikuihesabu lakini hii michezo minne ni freshi na ndio michezo inayohitaji maandalizi, Simba hata mkituamsha usiku sisi tunacheza nao, kwahiyo mechi ipo kama ilivyopangwa na bodi ya ligi.” Amesema Hassan Bumbuli.
Mchezo wa Simba SC na Young Africans ulipaswa kucheza Mei 08 mwaka huu, lakini uliahirishwa na Bodi ya Ligi kufautia sintofahamu ya kubadilishwa kwa muda wa kuanza kwake, uliokua umepangwa kucheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Awali mchezo huo ulipangwa kuanza mishale ya saa kumi na moja jioni, na baadae TFF na Bodi ya Ligi walitangaza kuupeleka mishale ya saa moja usiku, kwa kuweka wazi sababu za kuagizwa na mamlaka za Serikali.