Rais wa Shirikisho la soka nchini TFF Wallace Karia ameendelea kutoa ufafanuzi wa namna anavyosaidia soka la Tanzania pale anapohitajika kufanya hivyo, hususan katika ngazi ya klabu za Ligi Kuu na klabu nyingine za madaraja la chini.

Karia ametoa ufafanuzi huo, kufuatia sakata linaloendelea hivi sasa kuhusu Uongozi wake kuiminya Young Africans hasa inapokua na kesi kwenye kamati za TFF dhidi ya watani wao wa jadi Simba SC.

Kiongozi huyo amesema katika uongozi  wake amejitahidi sana kutenda haki na klabu moja wapo aliojitolea kuisaidia ni Young Africans, ambayo viongozi, wanachama na mashabiki wake hawachoki kumlaumu.

Amesema msaada aliowahi kuutoa kwenye Klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni kuivusha katika kipindi kigumu, ambacho iliwahi kupita, hasa baada ya kuondoka kwa aliyekua kiongozi na mfadhili Yusuph Manji.

“Baada ya Manji kupata matatizo na kuondoka, Young Africans ilipita katika wakati mgumu, nimeshirikiana na Sana kuisaidia klabu hii. Mimi ni Coastal si Young Africans, walikuwepo Tenga amecheza Young Africans, Malinzi alikuwa Katibu Mkuu wa Young Africans lakini hawakuifanyia Young Africans kama nilivyofanya mimi.”

“Ukienda mtaani utasikia watu watakwambia hakuna Rais wa TFF aliyeionea Young Africans kama Karia, lakini ukienda ndani ya TFF watakwambia hakuna mtu aliyeisaidia Young Africans kama Karia, kama mkiwapata viongozi wasema ukweli, watawaambia,”

“Siwezi kuifanyia mabaya Young Africans, hizi ni timu zinazoililetea heshima Taifa, mimi ninaheshimiwa huko nje kwa sababu ya Simba SC na Young Africans. Sisi wenyewe hatutambui ukubwa na heshima wanaotupa hawa mabwana kwenye ukanda wetu huu, hizi timu naziheshimu sana.”

Nigeria kubadili jina
Bumbuli: Nilikua natania