Wajumbe wa Bunge la juu la Ufaransa (SENATE) limeipongeza Tanzania kwa kuwa kinara wa masuala ya utulivu,amani,ulinzi na usalama katika eneo la maziwa makuu hususan katika maeneo ya Mashariki ya Kongo pamoja na eneo la Kaskazini mwa Msumbiji.
Wajumbe hao ambao pia ni kundi la Wabunge marafiki wa Tanzania wametoa pongezi hizo wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba n Kabudi alipotembelea Bunge hilo na kuongeza kuwa kupitia Jumuiya za kikanda ikiwemo SADC, Tanzania imekuwa kiongozi katika kuhakikisha amani kaskazini mwa Msumbuji na kwamba wajumbe hao wako tayari kuunga mkono jitihada hizo.
Wajumbe hao wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kujenga uchumi imara, na kusema wajumbe wa Bunge la juu la Ufaransa wako tayari kuhamasisha watalii wengi kutoka Ufaransa na Ulaya kuja Tanzania, ili kuifanya sekta ya utalii kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania.
Katika hatua nyingine Waziri Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), ambalo limeonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika masuala ya maendeleo vijijini ikiwemo nishati, maji na miundombinu.
Kwa upande wake Naibu Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo Bouduin Philippe ameipongeza Tanzania kwa kuingia katika uchumi wa kati miaka mitano kabla ya muda uliokuwa umepangwa na kuitaka Tanzania kuchukua hatua za kuimarisha huduma mbalimbali za maendeleo na uchumi hususani vijijini ili kuifanya hadhi ya uchumi wa kati kuonekana kwa wananchi wa kawaida.
Prof. Kabudi yupo Paris Nchini Ufaransa kwa ziara ya siku nne kufuatia mwaliko wa Waziri wa Ulaya na mambo ya Nje wa Ufaransa, ambapo pia anaitumia fursa hiyo kukutana na makundi ya wafanyabiashara pamoja na taasisi za serikali na binafsi za Ufaransa kuhamasisha masuala ya uwekezaji na biashara Tanzania.