Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema kuwa deni la Taifa linaongezeka kila mwaka ambapo kwa mwaka wa fedha ulioshia Juni 30, 2020 deni limeongezeka kwa kiasi cha shillingi Trillioni 3.65 sawa na asilimia 7 ikilinganiswa na deni lililoripotiwa mwaka 2018 / 2019.
CAG ameeleza hayo leo Aprili 8, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusiana na matokeo ya ukaguzi wa mahesabu kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2020 ambapo deni la serikali lilikuwa ni shilingi Trilioni 56.76, deni la ndani likiwa Trillioni 15.52 la nje Trilioni 41.24.
Amesema kuwa Ongezeko hilo la deni la taifa linajumuisha kiasi cha shilingi Bilioni 652 za deni la ndani na shilingi Trilioni 3 za deni la nje.
Aidha, Kichere ameelezea mwenendo wa hati kwa mwaka wa fedha 2019/ 2020 ambapo jumla ya hati za ukaguzi ni 900, kwa upande wa Serikali kuu hati zikiwa ni 243, mamlaka ya Serikali za Mitaa hati 185 , Mashirika ya Umma hati 165, miradi ya maendeleo hati 290, hati 17 za vyama vya siasa.
Ameongeza kuwa kati ya hati alizofanyia ukaguzi hati 800 ndIo hati zinazoridhisha sawa na asilimia 89, hati zenye shaka ni 81 sawa na asilimia 9, hati mbaya ni 10 sawa na asilimia moja na hati 9 hazikutolewa maoni sawa na asilimia moja.