Shirikisho la soka nchini Paraguay (APF) limemtangaza Kocha Juan Carlos Osorio, kuwa mkuu wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya nchi hiyo kuanzia jana jumatatu.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 57, aliiongoza Mexico wakati wa fainali za kombe la dunia, na kuifikisha katika hatua ya 16 bora nchini Urusi, kabla ya kuondolewa kwenye fainali hizo kwa kufungwa na Brazil mabao mawili kwa moja.
Osorio amewahi kuzinoa baadhi ya klabu nchini kwao Colombia, Mexico, Brazil na Marekani.
Alipewa mkataba wa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Mexico mwaka 2015, na baada ya kushindwa kufikia lengo katika fainali za kombe la dunia za 2018, alitangaza kujiuzulu.
Uongozi wa APF umesema kocha Osorio atakua na jukumu kubwa la kuiongoza Paraguay kwenye fainali za mataifa ya kusini mwa Amerika (Copa America) zitakazifanyika nchini Brazil mwaka 2019, na kisha kuiwezesha nchi hiyo kufuzu fainali za kombe la dunia mwaka 2022.
Mara ya mwisho Paraguay ilishiriki fainali za kombe la dunia mwaka 2010 zilizofanyika Afrika kusini.