Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amekosoa tamko lililotolewa hivi karibuni na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhusu tatizo la ukame nchini.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Polepole ambaye hakuwahi kumzungumzia Lowassa tangu aliposhika nafasi hiyo, alisema kuwa wananchi wanapaswa kumpuuza kiongozi ambaye ametangaza kuwa anafanya mpango wa kuwapa chakula cha bure.
Ingawa hakumtaja jina, hivi karibuni, Lowassa alieleza kuwa kwakuwa Serikali imesema haitagawa chakula yeye na chama chake cha Chadema wamekubaliana kutafuta msaada wa chakula kwa ajili ya wananchi.
“Lakini ametokea kiongozi mmoja anawaahidi kuwa ataenda kuwaombea chakula cha bure. Imeandikwa asiyefanya kazi na asile. Watanzania hawa wametutuma tuwawekee mazingira mazuri ili wafanye kilimo na biashara,” alisema Polepole.
“Kiongozi anayesema ataleta chakula cha bure na watu wasifanye kazi ni habati mbaya sana,” aliongeza.
Aidha, Polepole alisema kuwa wapo wanasiasa ambao wamekuwa wakitoa taarifa zisizo za kweli kuwa nchi inakabiliwa na baa la njaa bila kuzingatia uzito wa suala hilo. Alisema wanafanya hivyo bila kuwa na taarifa sahihi kwani hakuna baa la njaa nchini.
Alisema kuwa baa la njaa sio kitu kidogo na kwamba mwenye dhamana ya kutangaza kuwepo kwa tatizo hilo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli pekee.
Hivi karibuni, Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amekuwa akisisitiza kuwa serikali inapaswa kutangaza uwepo wa baa la njaa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Serikali imekanusha uwepo wa njaa nchini na kwamba kilichopo ni ukame katika baadhi ya maeneo ya nchi.