Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea na msimamo wake kudai vyombo vya uchunguzi kutoka nje viruhusiwe kuchunguza tukio la mbunge Tundu Lissu kupigwa risasi licha ya kutolewa ufafanuzi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.
Juzi, Mwigulu alieleza kuwa hakuna haja ya kutumia vyombo vya nje kuchunguza tukio hilo kwani vyombo vya usalama vya ndani ya nchi vina uwezo na weledi wa kutosha.
Aliongeza kuwa hata wataalam wa nje wakiruhusiwa bado watafanya kazi katika mazingira ya Kitanzania, kutumia sheria za Tanzania na kushirikiana na wataalam wa ndani ya nchi.
Mkurugenzi wa Itikadi na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema amepinga hoja za Waziri Mwigulu akidai kuwa kama hakuna hofu ni vyema wataalam wa nje waruhusiwe.
“Kwanini Serikali haitaki wachunguzi huru? Mrema alihoji. “Ni kweli kwamba wakija watafanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini hii haibadili msimamo wetu. Hawa wana vifaa na wanaweza kusaidia katika uchunguzi,” aliongeza.
Alisema kuwa Serikali bado haijatolea majibu uchunguzi juu ya tukio la kupotea kwa mwanachama wao, Ben Saanane pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, hivyo wana hofu kuwa huenda suala la Lissu pia likawa na sura hiyo.
Aliongeza kuwa tangu Lissu aliposhambuliwa kwa risasi Septemba 7 jeshi la Polisi bado halijaeleza kuwakamata watuhumiwa au hatua za uchunguzi zilipofikia.
“Kwahiyo, muafaka ni wachunguzi huru. Mtu hawezi kupigwa risasi mchana kweupe tena Dodoma Mjini,” Mrema aliliambia gazeti la Mwananchi.
Juzi, Waziri Mwigulu alieleza kuwa suala la uchunguzi halifanywi kwa siku moja na kwamba hata kama litachelewa lazima watuhumiwa wanaojificha kwenye kivuli cha ‘watu wasiojulikana’ watakamatwa.
Alitoa mfano wa msako wa Osama Bin Laden uliofanywa na Marekani kwa takribani miaka 10, lakini mwisho alipatikana na kuuawa.