Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila ameipongeza Timu ya Watalaam wa Afya kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa na wadau wa Kitaifa na Kimataifa kwa kuendelea kushirikiana na Mkoa kupambana na Ugonjwa wa Marburg.
Chalamila ametoa pongezi hizo katika kikao cha kamati ya Wajumbe Maalum wa kukabiliana na Ugonjwa wa Marburg kilichofanyika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera na kusema kazi inayofanywa na kamati hiyo ni kubwa na inasaidia kukabiliana na ugonjwa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila.
Amesema, “niwapongeze kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya na ninyi kutoka mashirika ya Kimataifa mmetusaidia sana kufikisha ujumbe uliosahihi na taswira ya nchi yetu kwa mataifa mbalimbali na ninachosisitiza ninyi wataalam wa afya lazima muwe na ujasiri wa kitaaluma.”
Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Issesanda Kaniki alitoa pongezi kwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kwa kuchukua hatua za haraka ikiwemo kutuma timu ya madaktari bingwa 12 walioweka kambi mkoani Kagera mara tu ugonjwa wa Marburg uliporipotiwa.