Uongozi wa klabu ya Young Africans umeeleza kusikitishwa na kifo cha mchezaji wake wa zamani Athumani Juma Chama maarufu kama ‘Jogoo’ aliyefariki katika Hospitali ya Muhimbili usiku wa kuamkia leo.
Akituma salamu za ramirambi kwa niaba ya Young Africans, Katibu Mkuu Charles Mkwasa amesema wamesikitishwa na kifo cha mkongwe huyo aliyewahi kutamba katika klabu hiyo miaka ya nyuma.
Amewataka wapenzi na wanachama wa Young Africans kuungana pamoja na familia ya marehemu Chama katika kipindi hiki kigumu.
Taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa marehemu Yombo Mwisho jijini Dar es salaam, ambapo anatarajiwa kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele kesho Jumanne katika makaburi ya Kisutu saa saba mchana, baada ya kuswaliwa katika msikiti wa Manyema.