Klabu Bingwa Barani Ulaya Chelsea FC ipo kwenye nafasi nzuri ya kumsajili Mshambuliaji kutoka nchini Norway na klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani Erling Braut Haaland.
Chelsea wanapewa nafasi hiyo ya kipekee kumsajili Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 20, kufuatia klabu nyingine ziliozkuwa na lengo la kumsajili kupunguza kasi ya kufanya hivyo.
Sababu kubwa ya klabu hizo kupungumza kasi ya kumuwania Haaland, ni ada kubwa ya usajili iliyowekwa na klabu yake ya Borussia Dortmund ambayo inakadiriwa kufikia Pauni Milioni 150.
Chelsea FC imeripotiwa kuwa tayari kutoa kiasi cha Pauni Milioni 150, ili kukamilisha mpango wa usajili wa Mshambuliaji huyo ambaye mpaka sasa ameshaifungia Borussia Dortmund mabao 40 katika michezo 43 aliyocheza.
Inadaiwa kuwa wawakilishi wa Chelsea FC walishafanya vikao kadhaa na wawakilishi wa Mshambuliaji huyo ili kuangalia uwezekano wa kumsajili na mambo yalikwenda vizuri kwenye majadiliano, hivyo kilichosalia ni utekelezaji.
Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City, walikuwa washindani wakubwa wa Chelsea katika dili la usajili wa Haaland, lakini wameamua kujitoa kutokana na fedha ya usajili iliyotangazwa.
Haaland alijiunga na Borussia Dortmund mwaka 2020 akitokea Red Bull Salzburg ya Austria kwa ada ya Euro Milioni 20.