China, Urusi na Cuba zimeshinda viti kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, licha ya upinzani kutoka kwa makundi ya wanaharakati kuhusiana na rekodi mbaya za mataifa hayo kuhusu haki za binadamu.
Urusi na Cuba zilikuwa zinawania bila upinzani, lakini China na Saudi Arabia zilikuwa katika kinyang’anyiro cha mataifa matano kwenye mchuano pekee wa kuwania nafasi kwenye Baraza la Haki za Binadamu.
Aidha Katika mchakato wa kura ya siri, ndani ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa, lenye wanachama 193, Pakistan ilipata kura 169, Uzbekistan 164, Nepal 159, China kura 139 na Saudi Arabia ilipata kura 90.
Licha ya mipango ya mageuzi iliyotangazwa na Saudi Arabia, shirika la haki za binadamu la Human Rights na mengine yalipinga ugombea wa Saudi Arabia yakisema taifa hilo la Mashariki ya Kati linaendelea kuwalenga watetezi wa haki za binadamu, wapinzani na wanaharakati wa haki za wanawake.
Aidha, yamesema Saudi Arabia imeonesha uwajibikaji mdogo kwa ukiukaji wa zamani, ikiwemo mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul nchini Uturuki, miaka miwili iliyopita.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pia lilizichagua Cote d’Ivoire, Gabon, Malawi, Bolivia, Ufaransa na Uingereza kwenye baraza la haki za binadamu lenye wanachama 47.
Senegal, Ukraine na Mexico zilichaguliwa pia kwa muhula wa pili wa miaka mitatu na wanachama wa baraza hilo hawawezi kuhudumu kwa zaidi ya mihula miwili.