Wakati Rais wa Marekani, Donald Trump akimuelezea kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un kama ‘kichaa anayemiliki makombora’, Shirika la Ujasusi la nchi hiyo (CIA) limetoa maelezo tofauti kuhusu akili na lengo la kiongozi huyo.
Mkurugenzi Msaidizi wa CIA katika oparesheni ya ukanda wa Korea, Yong Suk Lee amesema kuwa kuna sababu za wazi na lengo la Kim Jong Un kuichokoza Marekani na kuendelea na majaribio ya makombora ya nyuklia.
Lee amesema kuwa Kim Jong Un ndiye mtu anayependa zaidi mgogoro wa Penisula hiyo uendelee na kuitaka Marekani ‘kutomchukulia poa’ kiongozi huyo wa Korea Kaskazini au kufikiria kuwa ni kichaa tu.
Alisema kuwa Kim Jong Un anataka kutawala hadi kufa kwa amani katika taifa lake na kwamba ubabe wake dhidi ya Marekani na vitendo vyake vya kikatili dhidi ya wanaompinga ni mbinu yake muhimu zaidi.
“Kuamka asubuhi na kuishambulia Los Angeles kwa makombora ya Nyuklia sio kitu ambacho Kim Jong Un anataka kufanya,” alisema Lee. “Anataka kutawala kwa muda mrefu zaidi na kufa kifo cha amani kitandani kwake,” aliongeza.
Wazo hilo liliungwa mkono na Mkurugenzi Msaidizi wa CIA ukanda wa Mashariki ya Bara la Asia na Pacific, Michael Collins ambaye alisema sababu za msingi za uchokozi huo ni kuimarisha utawala wake ndani ya nchi hiyo kisiasa.
Tangu alipoingia madarakani mwaka 2011, Kim amekuwa na nguvu kubwa ndani ya nchi yake na kujiimarisha kijeshi huku akiibuka kuwa tishio kwa Marekani na marafiki zake kupitia mpango wake wa kujiimarisha kwa makombora ya nyuklia.
Hivi karibuni amedaiwa kuamuru watu 340 kuuawa ambapo kati yao 140 ni waliokuwa maafisa waandamizi wa jeshi la nchi hiyo, kwa sababu mbalimbali.
Mwaka 2013, aliamuru mjomba wake, Jang Song Thaek kuuawa akimtuhumu kufanya usaliti na uhaini. Alimtaja kuwa adui kwa watu wote nchini humo hivyo akauawa.
Hivi karibuni, Kim amekuwa katika vita ya maneno na Rais wa Marekani, Donald Trump akieleza kuwa ataachia makombora mengine makubwa zaidi ya kinyuklia kama majibu kwa kauli za Trump.
Trump amejibu akieleza kuwa Marekani itachukua hatua ambazo inapaswa kuchukua kukomesha vitendo vya Korea Kaskazini dhidi yake.