Kumia mshambuliaji machachari  wa kikosi cha Leicester City, Jamie Vardy kumemtia kiwewe kocha Claudio Ranieri ambaye amekiri kukosekana kwake ni pengo kubwa.

Kisha akaweka bayana wasiwasi wake wa kuendelea kuwa katika nafasi ya juu wakati huu ambao Vardy atakuwa nje ya dimba kwa kusema timu ipo katika wakati mgumu wa mpito.

Jamie Vardy amefanyiwa upasuaji mdogo wa mtoki hivyo utamfanya apumzike kwa wiki mbili.

Vardy amekuwa na makali msimu huu kutokana na kuongoza katika upachikaji mabao ambapo hadi sasa ana mabao 15 aliyoyafunga kwenye michuano ya Ligi Kuu England.

Meneja wa klabu ya Leicester City, Claudio Ranieri alisema, straika wake ameacha pigo kubwa kikosini, hivyo ni wakati wa vijana wake wengine kujipanga ili kuweza kutetea nafasi za juu.

Alisema ingawa kikosi kina wachezaji wengi mahiri, lakini ni ukweli usio na mashaka kuwa Vardy ni kati ya wachezaji tegemeo katika timu yake hiyo inayopambana kwa ajili ya kumaliza ikiwa katika nafasi za juu, ikiwemo kuweza kutwaa uchampioni wa premier msimu huu.

“Tulianza kwa kujipanga tangu mwanzo wa msimu, malengo ni kuendelea kuwa katika kiwango bora, hususan kutwaa ubingwa wa msimu.”

“Tukiwa na Vardy tunaweza kutimiza malengo kwasababu ni kati ya wachezaji tegemeo, lakini kuumia kwake ni dhahiri kusema ni pigo kwetu sote.”

“Ninaloweza kuangalia ni kwamba, nani wa kumwandaa kwa ajili ya kupambana kwa ajili ya kuifanya timu ibakie kileleni, lakini ni jambo la kusubiri kuona maana kila mchezaji yupo katika morari kubwa,” alisisitiza kocha huyo.

Kabla ya kujiunga na Leicester, Vardy aliichezea klabu ya Fleetwood Town.

Van Gaal: Marouane Fellaini Ni Wahapa Hapa
Kuondoka Kwa Benitez Kumewasikitisha Baadhi Ya Watu