Brazil imetinga hatua ya Robo Fainali ya Copa America, baada ya kushinda michezo mitatu ya Kundi B, lenye timu za Colombia, Peru, Ecuador na Venezuela.
Brazil ambayo ni mwenyeji wa fainali hizo, leo alfajiri iliifunga Colombia maboa 2-1 na kufikisha alama 9, zinazoendelea kuiweka kileleni mwa msimamo mwa Kundi B.
Kabla ya mchezo huo, Brazil ilishinda mabao 4-0 dhidiya Peru, baada ya kuichabanga Venezuela mabao 3-0, kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kundi B.
Mabingwa hao mara 9 wa Copa America wamebakisha mchezo mmoja dhidi ya Ecuador, utakaochezwa Juni 27, Uwanja wa Olímpico Pedro Ludovico, mjini Goiânia.
Upande wa Kundi A katika michuano hiyo, Argentina inaongoza kwa kufikisha alama 7, ikifuatiwa na Chile yenye alama 5, Paraguay inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 3.
Mabingwa wa kihistoria kwenye michuano hiyo Uruguay wanashika nafasi ya nne kwa kuwa na alama moja, huku Bolivia ikiburuza mkia wa kundi hilo kwa kutokua na alama yoyote.
Wakati huo huo wachezaji Neymar (Brazil), Eduardo Vargas (Chile), Ayrton Preciado (Ecuador) na Ángel Romero (Paraguay) wameendelwa kuchuana katika orodha ya wapachikaji mabao kwenye Fainali za mwaka huu, huku kila mmoja akifunga mabao mawili mpaka sasa.