Kocha wa Klabu ya Arsenal, Mikel Arteta amethibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona, hatua iliyosababisha sintofahamu kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.
Kutokana na hali hiyo, kikosi kizima cha kwanza cha Arsenal na wafanyakazi wengine wametengwa kwenye eneo maaluma kwa siku 12.
Klabu hiyo imesema kuwa itafanya kikao cha dharura mapema leo ili kuzungumzia mustakabali wa klabu hiyo. Hata hivyo, Arsenal imeeleza kuwa wanatarajia kutoshiriki michezo kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Katika hatua nyingine, Beki wa Klabu ya Manchester City, Benjamin Mendy amelazimika kutengwa kutokana na hofu ya kuwa na maambukizi ya Virusi vya Corona baada ya familia yake kugundulika kuwa na maambukizi ya virusi hivyo.
Klabu hiyo imetoa tamko ambalo hata hivyo haikutaja jina la mchezaji huyo, lakini imekiri kuwa mchezaji wake mwandamizi ametengwa kwa hofu ya Virusi vya Corona.
“Klabu yetu inafahamu kuwa mmoja wa mwaamilia ya mchezaji wake mwandamizi amelazwa hosptalini akiwa na dalili za ugojwa wa mfumo wa pumzi. Anaendelea na vipimo ambavyo ni pamoja na vya kirusi cha Covid-19. Hadi pale majibu yatakapotangazwa, mchezaji husika yuko kwenye eneo maalum la kutengwa,” imeeleza taarifa ya Manchester City.
Mchezo kati ya Man City na Real Madrid uliotakiwa kushuhudiwa Jumanne ijayo umeahirishwa baada ya wachezaji wa klabu hiyo ya Hispania kuwekwa kwenye eneo maalum la kutengwa. Hatua hiyo ilitokana na taarifa za kuwepo mchezaji wa mpira wa kikapu aliyeathirika na virusi vya Corona. La Liga pia imeahirishwa.