Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ametoka jela baada ya kulipiwa faini ya Sh. 40 Milioni iliyoamriwa na Mahakama ili kukwepa kifungo cha miezi mitano jela.

Msigwa alitoka jela jana jioni, saa chache baada ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Gerson Msigwa kueleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amemlipia Sh. 38 Milioni kati ya Sh. 40 Milioni alizopaswa kulipa.

Mkurugenzi huyo wa Ikulu ambaye alionesha viambatishi vya malipo ya benki aliambatana na ndugu wa Mbunge huyo ambao walisimulia jinsi walivyopokea msaada huo.

Akizungumza na waandishi wa habari Mzee Simon Msigwa aliyejitambulisha kama Kaka yake Mbunge Msigwa, alieleza kuwa baada ya kusikia ndugu yao anapaswa kulipa faini au kufungwa jela, wao kama ndugu walichangishana fedha lakini walifanikiwa kupata Sh. 2 milioni tu. Ameeleza kuwa waliamua kuomba msaada kwa Rais Magufuli ambaye aliwaongezea Sh. 38 Milioni.

“Ni malipo ya Mchungaji Peter Msigwa ambaye juzi hapa alikabiliwa na kesi na kwenda kufungwa, yeye na wenzake wa Chadema, sasa tunakwenda kufanya taratibu zote ili tukamilishe na tumchukue ndugu yetu… mimi ni Kaka yake Mkubwa, yeye kwangu ni Kayemba,” alisema.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itikadi, Uhusiano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kuwa hawana ushahidi wa malipo hayo akieleza kuwa wao kama chama wamelipa Sh. 100 Milioni kwa ajili ya kuwatoa viongozi wake watatu gerezani akiwemo Msigwa.

“Tumeshapeleka malipo mahakamani, tunasubiri risiti ya mahakama. Kama kuna mwingine amemlipia Mchungaji Peter Msigwa hatuna ushahidi na uhakika nao, kama chama Mahakama haijaturejeshea fedha za Msigwa kwamba amelipiwa mara mbili,” alisema.

Mchungaji Msingwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa wa Chadema, alikuwa miongoni mwa viongozi wanane wa chama hicho waliohukumiwa kwenda jela baada ya kukutwa na hatia kwenye makosa 12 kati ya 13 waliyokuwa wanashtakiwa au kulipa faini ya jumla ya Sh. 350 Milioni.

Kati ya viongozi hao, alikuwemo Dkt. Vincent Mashinji ambaye alihamia Chama Cha Mapinduzi, na chama hicho kilimlipia faini yake.

Corona: Kocha wa Arsenal aambukizwa, Beki wa Man City atengwa
Rais Magufuli amtolea Msigwa faini ya sh 38 Milioni