Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli amemchangia mbunge wa Iringa mjini wa  Chadema Peter Msigwa faini ya sh 38 milioni kati ya sh 40 milioni anazotakiwa kulipa mbunge huyo ili atoke jela baada ya hukumu iliyotolewa na Mahakama machi 10, 2020.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano Ikulu Gerson Msigwa ambaye amesema kuwa baada ya ndugu wa Msigwa kuchangishana na kukusanya milioni 2 waliamua kumuomba Rais Magufuli awasaidie ili waweze kumtoa ndugu yao ambapo Rais Magufuli aliamua kuwachangia kiasi hiko cha pesa.

Gerson Msigwa amesema kuwa Peter Msigwa na Rais Magufuli ni mtu na mpwa wake hivyo watu wasije kuwa na sintofahamu ya kwa nini Rais ameamua kumchangia kiongozi wa upinzani Peter Msigwa ambaye alipigwa faini ya shilingi milioni 40.

Hata hivyo Msigwa ni kati ya viongozi wanne wa Chadema waliohukumiwa kulipa faini ya sh 350 milioni pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa Chama hicho Dkt.Vicent Mashinji au kwenda jela miezi mitano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.

Mara baada ya Hakimu Mkazi Thomas Simba kusoma hukumu Chadema walianza kuchangishana fedha kwa ajili ya kuwalipia viongozi hao.

Hata hivyo Freeman Mbowe na wenzake walilazimika kwenda jela baada ya kushindwa kukamilisha taratibu ya kulipa faini hiyo waliyohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Aidha, baadhi wa wabunge kutoka Chadema tayari wametoka kupitia fedha zilizokusanywa na wanachama wa Chadema kufuatia kampeni inayoendeshwa na wanachama wa Chadema kukusanya kiasi hiko cha pesa ili waweze kuwatoa viongozi hao.

Viongozi waliofanikiwa kutoka jela ni Ester Bulaya (Bunda), Ester Matiku(Tarime mjini), na Halima Mdee(Kawe) huku baadhi ya viongozi wakiwa bado wapo Segerea akiwemo John Mnyika, Freeman Mbowe, John Heche, Peter Msigwa na Salim Mwalimu.

 

Msigwa atoka jela, ndugu zake waeleza JPM alivyolipa Sh. 38 Milioni, Chadema wang’aka
Lema ndani ya 18 za DPP