Katika harakati za kuunga mkono juhudi za Serikali za uboreshaji wa miundombinu ya elimu nchini, Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimekabidhi mifuko 300 ya saruji kwa halmashauri ya jiji la Dodoma, yenye thamani ya Shilingi Milioni 4,650,000.
Akikabidhi mifuko hiyo kwa niaba ya walimu, Katibu wa Chama cha walimu (CWT) Taifa Deus Seif, amesema hatua hiyo inatokana na kauli mbiu ya CWT ambayo ni “Wajibu na Haki”, na hasa ikizingatiwa kuwa wao ni sehemu ya maboresho ya elimu.
“Ni lazima tuhakikishe walimu wanakuwa katika sehemu salama kiufundishaji, na ni wajibu wetu kutoa mchango katika maendeleo ya elimu kwa sehemu mbalimbali, sasa hii ni sehemu tu ya uwajibikaji wenye lengo la kuboresha miondombinu ya elimu hapa nchini,” amesema Seif.
Aidha amesema utaratibu huo utaendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu, ili kuhakikisha uboreshwaji wa miundombinu hiyo nchini unafanyika kwa wakati na kwa ufanisi, na kusaidia kuleta matokeo chanya katika sekta ya ufundishaji na ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi.
Awali akipokea msaada huo, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Davis Mwamfupe, amesema CWT imeonesha mfano wa kuigwa, hivyo ni matarajio yake kitendo hicho kitaungwa mkono na mashirika, sekta mbalimbali, Serikali na taasisi nyingine, ili kuunga mkono juhudi za uboreshaji wa miondombinu ya elimu nchini.
“Na mifuko hii ya saruji ili tuone imefanya kazi ya matokeo chanya inatakiwa ielekezwe katika eneo moja na sio kugawa kwa shule zote kwa sababu itakuwa haifanikishi lengo, na kazi itakayofanyika CWT waitwe waone namna msaada walioutoa umefanya kazi kwa muonekano upi,” ameongeza Mwamfupe.
Kwa upande wake afisa elimu msingi wa Jiji la Dodoma Joseph Mabeyo, amesema Jiji lina mahitaji ya vyumba vya Madarasa 1522, na vilivyopo ni 916 pekee, huku mahitaji ya matundu ya vyoo kwa wanafunzi wa kiume yakiwa ni 1936, wakati yaliyopo ni 506.
“Pia mahitaji ya matundu ya vyoo kwa upande wa wanafunzi wa kike ni 2456 na yaliyopo ni 577 tu, hivyo upo uhitaji mkubwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali kukamilisha hili suala kwa mantiki ya kuchochea matokeo chanya ya kielimu,” amesema Mabeyo.