Msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, Rajab Abdul ‘Harmonize’ ameendelea kufanya vyema katika nyanja za kimataifa baada ya kutajwa katika tuzo za muziki za kimataifa.

Harmonize juma hili ameng’ara tena baada ya kutajwa kama mwanamuziki pekee kutoka Afrika Mashariki atakayewania tuzo kubwa za muziki barani Ulaya za MTV Europe Music Awards kwa mwaka 2019.

Mwaka 2019 vipengele vya Tuzo za MTV Europe Music Awards vimetangazwa na zitafanyika Novemba 3, 2019 jijini London nchini Uingereza ambapo Harmonize anashindanishwa na wanamuziki kutoka Afrika Magharibi.

Akizungumzia kuhusu suala hilo meneja wa msanii huyo Beauty Mmary  alisema ni nafasi nyingine kwa mwanamuziki huyo kung’aa kimataifa na kuwaomba mashabiki wake waendelee kumuunga mkono kwa kumpigia kura kwa wingi ili alete ushindi Tanzania.

“Ni jambo kubwa, tunaomba mashabiki na watu wote wanaopenda muziki huu ufike mbali, basi waendelee kumpa sapoti Harmonize ili tuzo ije Tanzania kwani ni heshima kubwa,” amesema Mmary

Mbali na Harmonize, wanamuziki wengine wanaowania tuzo hiyo kwenye Kipengele cha Best African Act 2019 ni Burna Boy, Teni, Nasty C, Prince Kaybee na Toofan.

 

Video: Hii ndiyo njia ya kuuza madini ya TIN nje ya nchi
CWT yaiunga mkono Serikali kuboresha Miundombinu ya Elimu