Matumizi ya njia mbalimbali za uzazi wa mpango yameongezeka katika mkoa wa Dar es Salaam mpaka kufikia asilimia 26 kutoka asilimia 13 mwaka 2018.
kauli hiyo imetolewa na , mratibu wa huduma za afya ya uzazi kwa vijana na jinsia kutoka Wizara ya Afya, Gerald Kihwele amesema iwapo mpango mkakati wa uzazi wa mpango kwa mwaka 2019/2023 utafuatwa nchini, unakadiriwa kupunguza mimba zisizotarajiwa 7,148,748, utoaji mimba holela 2,669,638 na vifo 22,164.
Hata hivyo, ongezeko hilo limetokana na uhamasishaji uliofanywa na Serikali kupitia utekelezaji wa mradi wa TCI- Tupange Pamoja uliofadhiliwa na mfuko wa Bill & Melinda Gates.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuzipongeza manispaa zilizofanya vizuri katika mradi huo, Meneja mradi kutoka shirika lisilo la kiserikali la Jhpiego, Rose Mnzava, alisema ongezeko hilo linaonyesha elimu imefika kwa jamii kama ambavyo mradi ulivyokusudia.
“Ukiangalia mwaka 2018 wakati tunaanza mradi huu, tulikuwa kwenye asilimia 13, hivi sasa mkoa umeshafikia asilimia 26 na wilaya ya Ubungo imejitahidi zaidi kwa kufikia asilimia 34 haya ni mafanikio,” amesema Mnzava.
Naye mratibu wa huduma za afya ya uzazi kwa vijana na jinsia kutoka Wizara ya Afya, Gerald Kihwele alisema kuna kila sababu kundi la vijana kupewa kipaumbele kupata huduma na kwamba lisibaguliwe.
“Kundi hili kuanzia miaka 10 hadi 24 lina haki ya kupewa elimu na huduma za afya za uzazi kwenye vituo. Hivi sasa Serikali inawawezesha watoa huduma kutoa huduma inayoendana na umri wa mtoto,” amesema Kihwele.