Aliyekua mlinda mlango wa klabu ya Arsenal kuanzia mwaka 1990 hadi 2003, David Seaman amemtaka mlinda mlango kinda wa klabu hiyo Bernd Leno kuendelea kuwa mstahimilivu.
Seaman ambaye alitumikia Arsenal katika michezo 400, amesema mlinda mlango huyo kutoka nchini Ujerumani bado ana nafasi kubwa ya kuwa chaguo la kwanza la meneja Unai Emery, ambaye alimsajili akitokea Bayer Leverkusen kwa ada ya Pauni milioni 22.5.
Amesema mpaka sasa anafurahishwa na mwenendo wa Leno, ambaye hajatumika katika mchezo wowote tangu msimu huu wa 2018/19 ulipoanza, na badala yake Petr Cech amekua chaguo la kwanza klabuni hapo.
“Leno anatakiwa kustahamili, ajifunze mambo mengi yanayohusu ligi ya England, ninaamini atakuwa mlinda mlango mzuri, tena chaguo la kwanza ambalo litadumu kwa muda mrefu,” alisema.
“Mpaka sasa ninafurahishwa na mwenendo wake wa kuwa kimya na kukubalia uhalisia wa mambo klabuni hapo, nafasi ya ulinzi wa lango aihitaji papara, inahitaji utulivu hasa unapojiunga na klabu inayoshiriki ligi ambayo hujaizoea.”
“Michezo bado ipo mingi na atakapopewa nafasi ninaamini ataweza kuonyesha kipaji chake na kila mmoja miongoni mwetu atamkubali. Leno ana umri mdogo sana, ukilinganisha na Cech, anakaririwa.”
Leno mwenye umri wa miaka 26, aliwahi kuandika katika ukurasa wake wa Teitter kuwa: “Ninaamini wakati wangu utafika, ninaendelea kujifunza kutoka kwa wenyeji wangu, kukaa kwangu nje tangu msimu umeanza hakumaanishi nimekuja hapa kutalii.”