Vyombo vya Habari Nchini, vimetakiwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya – DCEA, katika kuielimisha jamii juu ya athari za Dawa za kulevya kama sehemu ya mapambano ili kuepusha madhara kwa Taifa.
Wito huo, umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Taifa – TBC, Dkt. Ayub Rioba katika Semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini.
Amesema, “hii kazi siyo rahisi, licha ya Dawa hizi za kulevya kuwa ni tatizo la kihistoria lakini jitihada za pamoja zinahitajika kuhakikisha watumiaji na wauzaji hawapati nafasi popote katika jamii maana wana nguvu ya pesa na wanaweza kufanya lolote watakalo kama hatutakuwa wamoja.”
Amesema, usasa, kuiga watu mashuhuri, kushawishiwa na marafiki rika kijiweni na mitindo ya maisha imepelekea watu wengi kuingia katika mkumbo wa kutumia Dawa hizo za kulevya na kwamba athari za dawa hizo hupelekea Taifa kupoteza nguvu kazi, kuporomoka kwa maadili, kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu.