Nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz ametatua utata uliokuwepo wa kutokuwa na maelewano mazuri baina yake na aliyekuwa msanii wake chini ya WCB, Raymond Shabani ‘Rayvanny’ uliosababuishwa na masuala ya kimkataba.
Utata huo umeondolewa baada ya Chibu kutumia ukurasa wake ku ‘post’ picha ya Rayvanny iliyoambatana na ujumbe uliosomeka “Chui Young brother always!” za kumbukizi ya siku ya kuzaliwa mapema August 22, 2022.
Chapisho hilo la Diamond, limebatilisha uvumi kuwa nyota hao walitofautiana baada ya Rayvanny kuachana na lebo ya Wasafi na kujielekeza katika shughuli zake mwenyewe akisimamia rekodi label yake ‘Next Level Music’.
Wiki chache zilizopita, Rayvanny alidaiwa kutozwa faini ya Tsh 50 milioni kutokana na kuonekana kutumbuiza kwenye tamasha la Nandy kabla ya kuachana rasmi na WCB, lebo inayomilikiwa na Diamond Platnumz.
Taarifa za Vanny Boy, kulazimishwa kulipa faini hiyo zilienea kwa kasi zaidi baada ya dokezo lililotolewa na Watangazaji Mwijaku na Jose Mara, kufuatia mwimbaji huyo kuonekana katika ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa ‘BASATA’.
Kulingana na maelezo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Next Level Music hakuwa amemaliza mkataba wake kikamilifu kati yake na WCB Wasafi, kabla ya yeye kutokea ghafla kwenye tamasha la Nandy Festival.
Habari ambazo hazijathibitishwa, zinasema nyota huyo alitakiwa kulipa kiasi kisichopungua Tsh 800 Milioni kabla ya kuruhusiwa kuondoka rasmi WCB, na kupata haki zote za kazi zake alizofanya akiwa chini ya lebo hiyo.
Pamoja na kuenea kwa uvumi huo, Diamond Platnumz amejitokeza mara kadhaa kujibu madai ya kuwanyonya wasanii wake na kuwafanya kulipa kiasi kikubwa cha fedha ili kusitisha mikataba yao.
Katika mahojiano aliyofanya hivi karibuni, Platnumz alifafanua kuwa WCB Wasafi ni record label ambayo imewekeza fedha nyingi kwenye biashara ya muziki na atakayesainiwa chini ya lebo hiyo anatakiwa kuzingatia kanuni na masharti yaliyowekwa.